Friday, April 13, 2012

ATAKA JAMII ISIMHUKUMU MWANAWE, HAKI ITENDEKE, AELEZA USHIRIKA WA LULU NA KANUMBA Daniel Mjema



BABA mzazi wa msanii wa filamu, Elizabeth Michael 'Lulu,'

ATAKA JAMII ISIMHUKUMU MWANAWE, HAKI ITENDEKE, AELEZA USHIRIKA WA LULU NA KANUMBA
Daniel Mjema
BABA mzazi wa msanii wa filamu, Elizabeth Michael 'Lulu,' ameitaka jamii kutomhukumu mwanawe kutokana na kifo cha msanii mwenzake marehemu Steven Kanumba, badala yake iache vyombo vya sheria vifanye kazi yake.

Mzazi huyo, Michael Edward Kimemeta anayeishi mjini Moshi, amewaomba Watanzania kuiachia Mahakama iamue kama mtoto wao anahusika katika kifo hicho ama la.

Kimemeta, ameeleza kuwa binti yake ana umri wa miaka 16 tofauti na inavyoelezwa kuwa ana miaka 18.

Juzi Lulu alifikishwa katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka ya mauaji ya msanii mwenzake, Kanumba.

Kumekuwa na utata uliojitokeza kuhusu umri wa Lulu. Wakati mwenyewe akieleza kuwa ana miaka 17, Jeshi la Polisi lilieleza kuwa umri wake ni miaka 18 na juzi Mahakama iliambiwa kuwa msanii huyo ana umri wa miaka 17 na baba yake akisema ana miaka 16.

Kwa upande wake, mama mzazi wa Lulu Lucresia Karugila, alisema tukio la kifo cha Kanumba na kukamatwa kwa binti yake Lulu, limempa mshituko mkubwa na kumsababishia maradhi ya kisaikolojia na kimwili.

“Hayo yaliyotokea kwa kweli yamenifanya niumwe kabisa hapa sasa hivi nimelala naumwa…nimempa go ahead (ruksa), baba yake azungumze kwa sababu taarifa zote anazo. Naomba mimi mniache kwa sasa,”alisema.

Kimemeta aliliambia Mwananchi jana kuwa mwanawe huyo alizaliwa Aprili 17 mwaka 1995 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

“Nataka nikuambie (mwandishi) mwanangu atatimiza umri wa miaka 17 ifikapo Aprili 17 mwaka huu. Sasa ana umri wa miaka 16 na ni mtoto. Tunavyosikia Kanumba alikuwa mpenzi wake inatuuma sana,” alisema.

Baba huyo alisema alizaa na mama yake Lulu lakini hawakuwahi kuishi pamoja. "Mwanamke huyo alikuwa akifanya kazi Shirika la Ndege Tanzania (ATC) na muda wote Lulu alikuwa akiishi na mama yake jijini Dar es Salaam,"alisema Kimemeta.

Ameomba familia ya marehemu Kanumba ikubali kupokea pole ya familia ya Lulu kupitia gazeti hili kutokana na mazingira kutoruhusu familia hizo kukutana.

“Nasikitika mazingira ya tukio lenyewe mpaka sasa hayaruhusu familia yetu kwenda kutoa pole na kuifariji familia ya Kanumba kulingana na utamaduni wa mwafrika…tunaomba wapokee pole zetu kupitia njia hii,” alisema.

Kwa mujibu wa Kimemeta, hivi sasa wanahofia maisha yao kutokana na jamii kujenga mtazamo hasi juu ya tukio hilo hata bila ya kusubiri vyombo vya sheria kusikiliza ushahidi wa tukio hilo na kutoa hukumu yake.

Alisema kuwa jamii inapaswa ifahamu kuwa, kikatiba mtu yeyote anayeshitakiwa kwa kosa lolote haimaanishi tayari ni mkosaji, bali atahesabiwa kuwa mtuhumiwa hadi pale Mahakama itakapomtia hatiani.

“Yanasemwa mengi mara ooh Kanumba ndio alianza kumpiga mwanangu mara ooh Kanumba alisukumwa …mimi nasema tuiache Mahakama hata sisi hatupendi mtu auawe, lakini Mahakama iachwe itende haki,”alisisitiza.

Akizungumzia maisha ya mwanawe Lulu, Kimemeta alisema alipokuwa akitangaza Kipindi cha Watoto Televisheni ya ITV, walifarijika sana, lakini alipoanza kuingia kwenye sanaa ya filamu, walijua sasa wamempoteza.

“Baada ya kuingia kwenye sanaa ya maigizo niliona kabisa tumempoteza mtoto na nilimweleza mama yake kuwa wale aliokuwa nao katika maigizo akiwamo Kanumba mwenyewe, nilikuwa siwaamini hata kidogo,” alisema.

Kimemeta alidai kuwa siku moja mwanawe alimpigia simu akimwarifu kuwa alikuwa anakwenda jijini Arusha kurekodi filamu na Kanumba, yeye alipinga safari hiyo akitaka Kanumba amthibitishie usalama wa binti yake.

“Kwa sababu nilikuwa sipendezwi na hayo mambo nilimwambia mama yake azungumze na Kanumba na akatuhakikishia atamlinda na kambi yake ina maadili, lakini kumbe huo ndio ukawa mwanzo wa mwanaye kugeuzwa mpenzi wa msanii huyo,”alidai.


Elizabeth Michael 'Lulu,'

Baba huyo mzazi alidai kutofanya vizuri darasani kwa mtoto wake huyo, kulichangiwa na hatua ya kuingia katika sanaa ya uigizaji.


“Lulu alikuwa mtoto mwenye tabia nzuri sana hata alipokuwa ITV kwa kweli alitutia moyo wazazi wake kwa jinsi ITV walivyokuwa wakimlea, lakini alipojiingiza tu kwenye uingizaji hapo ndipo mambo yalipoharibika,” alisema.

Alikanusha madai kuwa mwanawe hakumaliza kidato cha nne na kusisitiza kuwa Lulu alisoma Shule ya Kimataifa ya St Mary's na baadaye alihamia Shule ya Sekondari ya Midway High School na kumaliza kidato cha nne mwaka jana.

Alisisitiza kuwa katika mambo yaliyokuwa yakiwaumiza mioyo, ni namna mtoto huyo alivyozidi kuharibika kwa kuingia katika fani ya uigizaji filamu.

Alisema angependa kukutana na Rais Jakaya Kikwete ili azungumze naye kama rafiki yake na watafute suluhisho la maadili kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.

Alisema tayari ameanza mchakato wa kuonana na Rais Kikwete ili amweleze siri aliyodai ni ‘nzito’ na kudai tayari ametafuta wazee watatu wenye busara wa kumsindikiza, endapo Rais atakubali ombi lake.

Pia ameziomba taasisi zinazojishughulisha na masuala ya haki za binadamu na msaada wa kisheria, kujitokeza na kumsaidia mwanawe.

Lulu alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam juzi na kusomewa shitaka la kumuua
Kanumba, tukio lililotokea Aprili 7 mwaka huu eneo la Sinza Vatican.

Msanii huyo hakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa Mahakama hiyo haina
mamlaka ya kusikiliza mashauri ya mauaji na hivyo alipelekwa rumande Gegeza la Segerea hadi Aprili 23 mwaka wakati kesi hiyo itakapotajwa.

Kifo cha msanii huyo kimetikisa nchi kutokana na umaarufu wake, akiwa ameigiza filamu 40 zilikuwa zikirushwa katika vituo mbalimbali vya
televisheni ndani na nje ya nchi.


Kanumba alipanga kujenga shule

Katika hatua nyingine, Fidelis Butahe na Pamela Chilongola wanaripoti kuwa mchaguaji maeneo ya kupigia picha za filamu za msanii Kanumba, Rahim Khatib alisema marehemu Kanumba alinunua eneo la ekari 15 huko Mpiji mkoani Pwani kwa ajili ya ujenzi wa shule yake ya sekondari.

Khatib alisema Kanumba alikuwa na mpango huo muda mrefu na kwamba lengo lake lilikuwa kuwasaidia wanafunzi wa eneo hilo ambao hutembea muda mrefu kutokana na shule kuwa mbali na eneo hilo.

“Kanumba alikuwa na mipango mizuri katika maisha yake, kuna eneo kubwa alilonunua Mpiji ili ajenge shule ya sekondari,” alisema Khatib.

Alifafanua kuwa hadi anafariki dunia, aliacha kiasi cha fedha zaidi ya Sh 40 milioni katika Kampuni yake ya Kanumba The Great.

“Marehemu ameacha fedha zaidi ya Sh 40 katika kampuni yake, magari matatu na hivi karibuni alinunua jingine aina ya Toyota Land Cruiser, ”alisema Khatib.

Katika hatua nyingine Khatib alisema kifo cha Kanumba ni pigo kwa watu waliokuwa wakifanya naye kazi akiwemo yeye mwenyewe kwa kuwa walikuwa wakimtegemea kwa kiwango kikubwa.

Sintah naye alonga

Kwa upande wake msanii maarufu wa filamu nchini, Christina Manongi maarufu kama Sintah ambaye alikuwa mmoja wa wasanii wa kwanza kufika nyumbani kwa marehemu Kanumba muda mfupi baada ya msanii huyo kuanguka, alisema kuwa siku tano kabla ya Kanumba kufariki, alikuwa na hasira tofauti na alivyomzoea.

Sintah ambaye alikuwa na msanii huyo katika Viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam Jumapili ya Aprili mosi pamoja na mwigizaji mwingine, Steve Nyerere alisema kuwa kila alichokuwa akimuuliza Kanumba, alimjibu kwa ukali.

“Ni tofauti na nilivyomzoea, siku ile ya Jumapili tulikaa pale Leaders Club mpaka usiku sana na kila jambo nililokuwa nikizungumza naye alinijibu kwa mkato na ukali kweli, ilinishangaza,” alisema Sintah

Alifafanua kuwa moja ya mambo waliyokuwa wakizungumza na Kanumba ni pamoja na yeye kutaka kuacha uigizaji, suala ambalo marehemu Kanumba hakuliunga mkono na kumjibu kwa ukali kuwa asijitoe katika uigizaji.

No comments: