Friday, May 4, 2012

SIMBA leo wanaanza kushangilia ubingwa wa Ligi Kuu

SIMBA leo wanaanza kushangilia ubingwa wa Ligi 
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya Azam FC
 kufungwa mabao 2-1 na Mtibwa Sugar kwenye
 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba ina pointi 59, ambazo sasa haziwezi kufikiwa 
na timu yoyote msimu huu na imebakiza mechi
 moja dhidi ya watani wa jadi, Yanga Jumapili 
ambayo kwao itakuwa ya kulinda heshima tu.
 Lakini Azam tayari imejihakikishia nafasi ya pili 
kwenye ligi hiyo na hivyo kukata tiketi ya kushiriki 
Kombe la Shirikisho la Soka Afrika mwakani.
Waliokuwa mabingwa watetezi Yanga, hawana tena 
chao- kwani hata wakiifunga Simba keshokutwa 
watabaki nafasi ya tatu tu, hivyo mwakani hawavuki
 mipaka ya nchi.

Tumaini pekee la Yanga kucheza michuano ya Afrika 
mwakani ni iwapo Simba SC itaingia hatua ya makundi
 ya Kombe la Shirikisho mwaka huu- ikiwa imebakiza 
mitihani miwili kufikia mafanikio hayo.
Inatakiwa kuitoa Al Ahly Shandy ya Sudan- na baadaye
 iitoe timu itakayokutana nayo kwenye mchujo wa 
kuwania kucheza hatua hiuyo, ambayo itakuwa
 imetolewa kwenye Ligi ya Mabingwa.
Hapo, Tanzania itakuwa na nafasi mbili kwenye 
Kombe la Shirikisho mwakani, kwa mujibu wa 
anuni mpya za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Tayari Simba imeifunga Shandy mabao 3-0 katika
 mchezo wa kwanza na inahitaji sare katika mchezo
 wa marudiano wiki ijayo ili kusonga mbele.

Katika mchezo wa leo, hadi mapumziko, tayari Mtibwa 
walikuwa wanaongoza kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani 
na Awadh Issa dakika ya 25, wakati kipindi cha pili, 
Wakata Miwa hao wa Manungu waliokuwa wanashangiliwa 
kwa nguvu na mashabiki wa Simba, walipata bao la pili
 dakika ya 59, mfungaji akiwa ni Juma Abdul.

Awadh alifunga bao lake akiunganisha kona iliyochongwa
 na nyota wa mchezo wa leo, Juma Abdul ambaye naye 
alifunga bao la pili kwa mpira wa adhabu, baada ya 
Luckson Kakolaki kumchezea rafu Vencent 
Barnabas Saramba. John Raphael Bocco aliifungia
 Azam bao la kufutia machozi.

No comments: